TAASISI ZA SEKTA YA MAJI TABORA ZAKUTANA NA WAHESHIMIWA WABUNGE WA MKOA WA TABORA
Taasisi za Sekta ya Maji Mkoa wa Tabora zimekutana na Wabunge wa Mkoa wa Tabora katika kikao kilichofanyika tarehe 16 April 2026, kikao hicho ambacho kwa utaratibu hufanyika kila mwaka, kimefanyika katika ukumbi wa Mkandarasi Place uliopo jijini Dodoma.

Lengo kuu la kikao hicho ni kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Tabora kuhusu kazi zilizotekelezwa na Sekta ya Maji Mkoa wa Tabora miaka mitano (5) iliyopita, mipango iliyopo na bajeti kwa mwaka wa fedha 2026/2027.Taasisi zilizoshiriki katika kikao hicho ni Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingira Mijini ambazo ni Tabora (TUWASA), Nzega (NZUWASA), Igunga (IGUWASA) na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutoka wilaya za Igunga, Uyui, Sikonge, Nzega, Urambo na Kaliua pamoja na Bonde la Ziwa Tanganyika.

Akitoa maelezo ya utangulizi, Meneja wa RUWASA mkoa wa Tabora Eng. Hatari Kapufi alieleza kuwa, Sekta ya maji Mkoa wa Tabora imefurahishwa sana na mwitikio wa Waheshiwa Wabunge kuhudhuria katika kikao hicho.
Taarifa ziliwasilishwa kwa njia ya Makala za picha mjongeo kwa Taasisi zote na hatimaye kuruhusu maswali na ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge.

Waheshimiwa wabunge wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wabunge Mkoa wa Tabora Mhe. Magreth Sitta, waliipongeza Sekta ya maji Tabora kwa utamaduni wake wa kukutana na Waheshimiwa Wabunge wa Tabora kwa lengo la kuwapitisha kwenye miradi mbalimbali iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa pamoja na mipango iliyopo. Aidha, kwa kuzingatia kuwa Wabunge wengi waliopo kwa sasa ni wageni, kikao hicho ni muhimu sana kwao maana kinawapatia ufahamu mkubwa wa kazi za maji katika majimbo yao.

Waheshimiwa Wabunge walipata muda mzuri wa kuuliza maswali na baadaye kupokea majibu na ufafanuzi kutoka kwa Wataalam wa sekta ya maji Tabora.
Wabunge wa Tabora wameshukuru kwa ushirikiano uliopo na Sekta ya maji na wameelekeza kuendelea kusimamia vema Taasisi hizo na kuahidi kutoa ushirikiano katika kuwezesha upatikanaji wa fedha za miradi pamoja na malipo ya Ankara za maji kwa wakati ili Taasisi za Maji mkoa wa Tabora ziweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Wabunge Mkoa wa Tabora, Mama Magreth Sitta, ameishukuru Sekta ya maji Tabora na kuisihi iendelee na utaratibu huo wa kuwashirikisha Waheshimiwa Wabunge.
Naye msimamizi wa sekta ya Maji Mkoa wa Tabora Eng. Hatari Kapufi aliwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa Mahudhurio pamoja na maswali, maoni na ushauri walioutoa. Aliahidi kuendelea kutekeleza maelekezo ya Viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge katika kufanikisha malengo yaliyowekwa.

