AWESO NA ILE NDOTO YA 2020.

AWESO NA ILE NDOTO YA 2020. NI SUALA LA MUDA TU, TABORA WATASHUHUDIA.

NA, EVARISTY MASUHA

Mwishoni mwa mwezi Julai 2020 nilibahatika kufanya mazungumzo na Waziri wa Maji Mhe Jumaa Aweso (Mb) wakati huo akiwa Naibu Waziri wa Maji, kwa cheo chake cha kazi, na uwaziri wake hata haukumfanya awe mbali kwamba ashindwe kujichanganya na kuongea mawili matatu, katika jamii yetu hii ambayo kila kukicha mengi yanajiri. Kwa wale wa Mkuranga mtakumbuka tukimuita “Ticha J” kwa kujitoa kwake kutuinua katika elimu.

 Swali langu lilikuwa kutaka kujua hatma ya huduma ya huduma ya maji katika wilaya zote za mkoa wa Tabora hasa baada ya huduma hiyo kufikishwa katika miji ya Igunga, Nzega na Manispaa ya Tabora. Takribani miaka mitatu sasa tangu mazungumzo yale yafanyike nimepata tena fursa ya kutembelea mkoa wa Tabora. Lengo likiwa lile lile tulilochati na Mhe. Aweso, kuthibitisha iwapo ndoto yake imetimia.

Safari yangu imeanzia ofisini kwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) hadi pori la Kijiji cha Maswanya kilichopo Uyui mkoani Tabora.

Nakumbuka Mazungumzo yangu na Mhe. Aweso ya mwaka huo wa 2020 yalitokana na mazungumzo yangu ya awali na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa wakati huo Mhe. Aggrey Mwanri, naamini bado twamkumbuka haswaa Mzee wa “Injinia soma hiyo”, pamoja na mazungumzo na baadhi ya wananchi wa wilaya za mkoa wa Tabora ambazo hazikuwa na huduma ya majisafi na salama.

Mazungumzo yangu na Mhe. Mwanri ambaye bado anaendelea kukumbukwa kwa kuutangaza mkoa wa Tabora kama Toronto ya Afrika yalifanyika juu ya  tenki la maji la Itumba lililoko mjini Tabora ukipenda “Tembo wa Tabora” akinionesha fahari ya Tabora, Toronto ya Afrika. Akasema ujio wa maji ya ziwa Victoria na jitihada za serikali zinazofanyika kuhakikisha maji haya yanasambazwa kila eneo la mkoa huo linaileta Toronto ya kweli ambayo wengi walidhani ni masihara.

Alishukuru timu  nzima ya Wizara ya Maji na serikali kwa ujumla kwa kuhakikisha huduma hiyo ya majisafi na salama inamfikia kila mwananchi wa Tabora. Sehemu ya mazungumzo yangu na Mheshimiwa Mwanri rejea yake inapatikanana katika kiungo cha channel ya youtube, majiDigital anuani Maji ya ziwa Victori mjini Tabora ni ishara ya Tabora kuwa Toronto - RC Mwanry - YouTube

Naibu Waziri Mhe. Aweso wakati huo, alinihakikishia kuwa hakuna mwananchi ambaye atapitwa na huduma ya majisafi na salama na kwamba watakaojaliwa kuwa hai ndani ya miaka mitano watashuhudia mageuzi na habari njema kabisa. Mhe. Aweso alirejea maneno yake ambayo amekuwa akiendelea kuyasema akinukuu kitabu cha Tenzi za Rohoni yasemayo ‘unapozuru wengine usinipite mwokozi’. Akasema Tabora ni njia ya kuelekea mkoa wa Mwanza ambako mradi wa maji wa ziwa Victoria unaanzia.

“Sitathubutu kuwapita wananchi wa Tabora na wilaya zake zote katika kuhakikisha maji ya ziwa Victoria yanawanufaisha” alisema Mheshimiwa Aweso, akaenda mbali zaidi kwa kuahidi kuwa si wananchi wa Mkoa wa Tabora tu bali wananchi wote wanaozungukwa na ziwa Victoria Mungu akimjalia nguvu na afya na kuendelea kuaminiwa na mamlaka katika nafasi aliyoaminiwa ndani ya Sekta ya Maji, atahakikisha huduma hiyo inamfikia kila mwananchi.

Sasa ni takribani miaka mitatu tangu Mzee Mhe. Mwanri astaafu. Ni takribani miaka 3 tangu Waziri Aweso apewe dhamana ya Uwaziri wa Maji. Nimepata fursa ya kutembela tena mkoa huu kwa lengo hilohilo la kujifunza mabadiliko yaliyopo na hata kujihakikishia iwapo Toronto ya Mwanri inaendelea. Iwapo wananchi wa mkoa wa Tabora hawajapitwa, nimekuwa kama yule “Tomaso” ila sio kwa ubaya.

Fursa hii imeniwezesha kuzungumza na viongozi wenye dhamana ya kuhakikisha majisafi, salama na yenye kutosheleza yanafikishwa kwa wananchi. Mhandisi Mayunga Kashilimu ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora kwa kifupi ikijulikana kama TUWASA.

Mhandisi Mayunga ananihakikishai kuwa hadi kufikia Oktoba 2025 wilaya zote za mkoa wa Tabora zitakuwa zimefikiwa na huduma hiyo. Anasema mkoa wa Tabora unajumla ya wilaya saba. Wilaya ambazo hadi sasa zimefikiwa na huduma ya majisafi na salama kutoka ziwa Victoria ni Igunga, Nzega, Tabora na Uyui.

Anaanza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa uthubutu wake wa kutenga fedha ili kuwezesha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa Tabora. Anamshukuru Mheshimiwa Aweso kwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha fedha hizo zinafika kwa wakati na usimamizi unakuwa thabiti ili kuhakikisha tamani ya fedha inaonekana kupitia utekelezaji wa miradi hiyo.

Anasema, kwa sasa mradi wa maji wa miji 28 unaendelea kutekelezwa na kwamba mradi huo unasambaza mabomba yenye urefu wa kilometa 190 ambazo zitawezesha miji yote ya makao makuu ya wilaya 3 ambazo hazijafikiwa na huduma ya majisafi kutoka ziwa Victoria zinafikiwa. Miji hiyo ni Urambo, Sikonge na Kaliua.  Mradi huu unatekelezwa na kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 62.2 na unatarajia kuhudumia wakazi zaidi ya 435,811. Aidha mradi huu utahudumia vijiji vyote vinavyopitiwa na miundombinu ya mradi na kuleta uhalisia wa mawazo ya Waziri Aweso ya kutompita mwananchi yeyote wa mkoa wa Tabora aliyeko katika eneo la mradi.

Mhandisi Mayunga anasema kwa sasa huduma ya maiisafi na salama katika Manispaa ya Tabora imefika asilimia 95 na bado wanaendelea kusambaza miundombinu ili kuhakikisha huduma hiyo inawafikiwa wananchi kwa asilimia mia moja.

Anakiri kuwepo na changamoto ya huduma ya maji katika baadhi ya miji anayoihudumia ambayo ni mji wa Sikonge ambao kwa sasa huduma hiyo imefikia asilimia 42.5. Mji wa Urambo uko asilimia 24.5 na asilimia 50 katika mji wa Kaliua.

“Niwahakikishie wananchi wa maeneo yote hayo kwamba taabu wanayopitia sasa ni ya muda tu kwani mradi huu unategemea kupandisha huduma ya maji hadi kufikia asilimia 95. Tuombe uzima tu.” Mkurugenzi Mhandisi Mayunga anasema

Kuona ni kuamini. Kutoka ofisini kwa Mkurugenzi wa TUWASA safari yangu imeniwezesha kwenda hadi pori la Kijiji cha Maswanya Wilayani Uyui ambako mkandarasi kampuni ya Mega Engineering and Infrastructure LTD anaendelea na shughuli ya kutandaza mabomba mradi wa maji wa miji 28. Safari hii siko peke yangu. Nimeambatana na Mkurugenzi Mhandisi Mayunga. Pamoja na kwamba sikubahatika kuonana na msemaji wa kampuni inayotekeleza mradi, kazi inaonekana kwenda kasi kwani kazi ya kuchimba mitaro inakwenda sambamba na kazi ya kutandaza mabomba.

Mhandisi Mayunga ananihakikishia kuwa yeye binafsi amezungumza na  mhandisi mshauri kampuni ya WAPCOS  na mkandarasi. Pia waziri Aweso amezungumza nao na kuwataka wakamilishe mradi kwa wakati kwani hakutakuwa na muda wa nyongeza.

Anasema zama za kurudi mezani kuanza kuzungumza na mkandarasi kuongeza muda wakati yeye mwenyewe aliahidi kuikamilisha kazi katika muda uliopangwa zimeisha. Lazima kazi ikamilike kwa wakati. Wananchi wapate huduma.

Kila laheri wananchi wa Tabora. Kila laheri Sekta ya Maji. Muendelee kunena na kutenda. Taifa linawategemea katika kumtua “mama ndoo ya maji kichwani”. Kweli kuona ni kuamini, mapinduzi ni makubwa, na hongera na pongezi kwa wote, manake usipokuwa na shukrani hata mazuri unayaharibu.

 

Evaristy Masuha

0717697205

Masuha8@gmail.com

Shughuli ya Uchimbaji wa Mtaro na usambazaji wa mabomba mradi wa maji wa Miji 28 unaendelea katika pori la Maswanya wilayani Uyui, Mkoani Tabora

Mkurugenzi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora Mayunga Kashilimu akizungumza na mwandishi wa Makala hii katika eneo la pori la Kijiji cha Maswanya, Wilayani Uyui Mkoani Tabora