KAMATI YA ULINZI NA...
KAMATI YA ULINZI NA USALAMA YA WILAYA YA URAMBO YAKAGUA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI WA MIJI 28.
18 Mar, 2026
KAMATI YA ULINZI NA USALAMA YA WILAYA YA URAMBO YAKAGUA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI WA MIJI 28.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Urambo Tabora, imekagua Utekelezaji wa Mradi wa Majisafi wa Miji 28 unaoendelea kutekelezwa katika eneo la Ilani, kata ya Muungano iliyopo wilaya ya Urambo.

Lengo la Ziara hiyo ni kukagua Utekelezaji wa Maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) alipotembelea mradi huo mapema Februari 7, 2026 ambapo alitoa maagizo ya kukamilisha mradi kwa haraka.

Akieleza hatua ya mradi na utekelezaji wa Maagizo ya Mhe. Waziri, Msimamizi wa Mradi wa Miji 28 Tabora Mha. Betty Kaduma kutoka KASHWASA amesema mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilioni 143 ukijumuisha Miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua, unaotekelezwa na Mkandarasi Megha Engineering & Infrastructure Ltd upo katika hatua za mwishoni na umefikia asilimia 76.5 ya utekelezaji wake.

Ameeleza kuwa ulazaji wa bomba kubwa kutoka Tabora kwenda katika Tanki la Muungano umekamilika tarehe 17 Machi 2026.   Ujenzi wa tangi la majisafi umefikia asilimia 85 ya utekelezaji wake na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi, 2026 ambapo maji yatajazwa katika tanki hilo.

Meneja wa TUWASA- Urambo Petro Kisasi amesema Wizara ya Maji imetoa fedha kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kupeleka maji mjini Urambo na tayari uzalishaji wa mabomba hayo unaendelea kiwandani. 

Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Urambo ambaye pia na Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Mhe. Dkt. Gerald Mongella ameipongeza TUWASA kwa Usimamizi mzuri wa Mradi na kusisitiza Utekelezaji ukamilike kwa haraka, bila kuathiri ubora wa mradi ili hatimaye uweze kuwafikia wananchi, kwani hayo ndiyo matarajio ya Mhe. Waziri.

Kukamilika kwa Mradi huu kutanufaisha jumla ya wakazi 490,926 katika maeneo ya Sikonge, Urambo na Kaliua ambao unatarajiwa kuongeza uzalishaji kwa lita 24,760,000 kwa maeneo yote kwa siku.