MKURUGENZI MTENDAJI WA MAMLAKA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA TABORA (TUWASA) MHA. MAYUNGA KASHILIMU AMETEMBELEA KITUO CHA KUCHOTEA MAJI KILICHOPO KATA YA MBUGANI
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) Mha. Mayunga Kashilimu ametembelea kituo cha kuchotea maji kilichopo Mbugani Texas kukagua hali ya usimamizi na uendeshaji wa Magati ya Maji.

Amehimiza usimamizi mzuri wa Magati ya Maji, kuhakikisha msimamizi wa kituo anakuwepo muda wote katika eneo la kituo kuepuka upotevu wa Maji. Halikadhalika kuweka bei za maji katika magati ya maji na kulipa kwa wakati fedha zinazopatikana kutokana na mauzo ya maji katika Magati hayo.

Benard Biswalo Mkurugenzi wa Idara ya huduma kwa wateja amemsisitiza Mwenyekiti wa Mtaa wa Sukuma Ndg. Juma Rehani kuhakikisha taratibu za upatikanaji wa wasimamizi wa magati ya maji zinafuatwa ikiwemo kusaini mikataba ya makubaliano hayo kati ya wasimamizi wa Magati ya maji na TUWASA.
Lengo ni kuhakikisha wateja wananunua maji kwa bei elekezi ambayo ni shilingi 30 kwa ndoo 1 ya lita 20 na kuimarisha usimamizi kwa kuwapa elimu wasimamizi wa Magati ya Maji.

