KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026 ARIDHIA KUWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA MAJI URAMBO
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Ndg. Wazo Michael Mwang'onda ameridhia na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa dharura wa Ujenzi wa Bomba la Usambazaji maji HDPE 110mm kutoka tanki kuu la Muungano (lita 2,000,000) kwenda urambo mjini Urambo tarehe 16/09/2026.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji TUWASA Benard Biswalo akisoma taarifa ya Mradi ameeleza Mradi huu wa dharura na ni ombi la Mhe. Magreth Sitta (Mb) kwa Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) alipotembelea mradi wa Miji 28 mwezi Februari 2026, kuwawezesha wakazi wa Urambo kupata maji ya ziwa Viktoria wakati wakisubiri kukamilika kwa Mradi mkubwa wa maji wa Miji 28.
Mhe. Aweso aliridhia na kuahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 500 ili kuanza mara moja kwa utekelezaji wa Mradi. Mpaka kukamilika kwake, mradi unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi 906,200,000. Aidha mradi umefikia asilimia 84.62 ya utekelezaji na unatarajiwa kunufaisha wakazi 17,446 wa mji wa Urambo.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru amesema amefurahishwa sana na usambazaji wa maji kwa wananchi kwani ni utekelezaji wa ahadi yake Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo kichwani. Aidha amewataka wananchi kutunza miundombinu ya maji ili iweze kutumika sasa na vizazi vijavyo, pia amesisitiza kuendelea kuimarisha amani na utulivu ili kuleta maendeleo.
Naye Mbunge wa Urambo Mhe. Magreth Sitta amemshukuru sana Mhe. Rais kwa kuleta maji ya ziwa Victoria kupitia Mradi wa maji wa Miji 28 kwani umetatua changamoto kubwa ya maji iliyokuwepo Mjini Urambo.

