NAIBU WAZIRI WA MAJI...
NAIBU WAZIRI WA MAJI ENG. MARYPRISCA MAHUNDI ATANGAZA NEEMA YA MAJI KWA WAKAZI WA URAMBO TABORA. AMTAKA MKANDARASI KUONGEZA KASI ZAIDI.
30 Jan, 2024
NAIBU WAZIRI WA MAJI ENG. MARYPRISCA MAHUNDI ATANGAZA NEEMA YA MAJI KWA WAKAZI WA URAMBO TABORA. AMTAKA MKANDARASI KUONGEZA KASI ZAIDI.

NAIBU Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amemtaka Mkandarasi wa Mradi wa Maji wa Miji 28 kuongeza kasi na nguvu ya utekelezaji wa mradi huo ili wananchi wapate maji haraka na kuondokana na adha ya ukosefu wa maji.

Mhandisi Mahundi ametoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi ya Maji Januari 23, 2024 katika Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora ambapo ametembelea mradi wa maji wa miji 28  ikiwemo kijiji cha Ndono ambapo bomba la kupeleka maji Urambo linapojengwa.

Aidha, Mhandisi Mahundi amewahakikishia wana Urambo kuwa  ifikapo mwezi Oktoba  2025 wananchi wa Urambo watapata Maji safi na salama yatokanayo na mradi huo wa maji  wa miji 28 unaotoa maji kutoka ziwa Victoria utakaogharimu kiasi cha shilingi Bilioni 145.

Mhandisi Mahundi alisema, "Wananchi hawa wa Urambo watanufaika na maji kutoka katika bwawa la Kalemela linalojengwa lenye thamani ya shilingi Bilioni 5 na niwahakikishie mpaka ifikapo mwezi Oktoba changamoto ya maji hautakuwepo eneo hili"

Kadhalika, Mhandisi Mahundi amewapongeza  Mkurugenzi wa TUWASA Eng. Mayunga Kashilimu, Meneja wa RUWASA Mkoa Eng. Hatari Kapufi, Mameneja wa RUWASA Wilaya zote za Tabora na watumishi wote wa Maji Mkoa wa Tabora kwa kazi wanayofanya ya kuhakikisha wanasambaza maji kwa wananchi  wa mkoa wa Tabora, kwa  kushirikiana na viongozi wa Serikali na  Chama cha Mapinduzi na kuwashirikisha wananchi katika huduma ya maji na utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo yao.

Wakitoa Taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo ya maji TUWASA na RUWASA wamemueleza Mhandisi Mahundi  kwamba utekelezaji wa mradi kuelekea Urambo eneo la Ndono umesimama kutokana na hali ya mvua na  kwamba maeneo mengine ujenzi unaendelea.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Urambo Kamishna Elibariki Bajuta ametumia wasaa huo kuelezea kuhusu kupungua kwa kasi ya ujenzi kwa mkandarasi  wa mradi huo kuwa ni pamoja  na hali ya mvua zinazoendelea kunyesha hapa nchini  na  kwamba mitambo ya ujenzi inazama na tope.