MKUU WA WILAYA YA URAMBO ASHUHUDIA UPOKEAJI WA MABOMBA YA MRADI WA USAMBAZAJI MAJI URAMBO
Mkuu wa wilaya ya Urambo Mhe. Dkt. Khamis Mkanachi ameshuhudia upokeaji wa mabomba ya Mradi wa usambazaji maji, kutoka tenki kuu la Muungano kwenda mjini Urambo kupitia mradi wa maji wa Miji 28, katika hafla iliyofanyika Boma Village mjini Urambo tarehe 2 June 2026.
Mabomba hayo ni ahadi iliyotimizwa na Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ambaye aliahidi kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 500 ili kukamilisha mradi, alipotembelea mradi huo mapema februari 7, 2026.
Katika hafla hiyo Dkt. Mkanachi ambaye alikuwa Mgeni rasmi akiwa na Mbunge wa Urambo wamepata fursa ya kutembelea maeneo ambapo mradi unaendelea kutekelezwa na kushuhudia maji ya ziwa Viktoria yakiwa yameshajazwa katika Tanki la Muungano, uchimbaji wa mitaro, ulazaji wa mabomba na uungaji wa mabomba ukiwa unaendelea.
Akielezea furaha yake Dkt Mkanachi amesema tukio hili linatengeneza historia, kwani wameshuhudia maji ya ziwa Viktoria yakiwa yamejazwa tayari kwenye tanki. Ameahidi kutoa ushirikiano kuongeza nguvukazi ili mradi ukamilike haraka kukamilisha ndoto ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.

Mbunge wa Urambo Mhe. Magreth Sitta amempongeza Mkurugenzi wa TUWASA na wahandisi wa maji Urambo kwa ushirikiano, amemshukuru Waziri wa Maji Mhe. Jumaa H. Aweso halikadhalika Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mha. Mwajuma Waziri kwa kutimiza ahadi yao ya kufikisha maji Wilaya ya Urambo. Amehimiza wananchi kutumia fursa hizo kufanya kazi kwa moyo kwa manufaa yao wenyewe.
"Wananchi tumuunge Mkono Mhe. Waziri wetu wa Maji kwa kutumia maji haya ya ziwa Viktoria mara tu yatakapofika" Hayo ameyasema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wakati akihamasisha wananchi kutumia maji hayo yanayoletwa kwa gharama kubwa na Serikali na kuahidi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA Mha. Mayunga Kashilimu amesema fedha zilizoahudiwa na Mhe. Waziri tayari zimefika, kazi yetu sasa ni kutekeleza mradi na kuhakikisha wananchi wanapata maji. Amewasihi wananchi kushiriki na kutoa ushirikiano katika kutekeleza mradi huo.
Utekelezaji wa mradi unahusisha ununuzi wa mabomba 1,750 ya urefu wa kilomita 21, kuchimba na kufukia mitaro, kununua viungio, kukata na kurejesha barabara za lami na njia za reli.
Mhe. Waziri ametoa fedha hizo ili kuanza kuleta maji katika mji wa Urambo wakati wakisubiri kukamilika kwa bomba kubwa litakalojengwa na Mkandarasi wa Miji 28 M/S Megha Engineering. Hadi kukamilika kwake, mradi unakadiriwa kutumia jumla ya shilingi 906,200,000.

