KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2026 AWEKA JIWE LA MSINGI MRADI WA KUFUNGA MITA ZA MALIPO KABLA
Ndg. Wazo Michael Mwang'onda ameweka jiwe la Msingi kwenye Mradi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira TABORA (TUWASA) wa Kufunga mita za malipo kabla kwa wateja tarehe 21/09/2026
Ameeleza kufurahishwa kwake na mradi huu wa Kufunga mita za malipo kabla ambao unamwezesha mteja kununua kiasi anachotaka na kwa wakati anaotaka. Amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya maji na ameipongeza TUWASA kwa kutekeleza maelekezo ya Mhe. Rais kwa vitendo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA Benard Biswalo akisoma taarifa ya mradi amesema Mradi huu ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa Wizara ya Maji kuanza kutumia mita za Malipo kabla. Ameeleza lengo ni kuwafungia mita hizi wateja wake wote. na amewaasa wateja kuwa waaminifu kulipa Ankara zao za maji kwa wakati ili kuiwezesha TUWASA kufikia lengo hilo.
Mita za malipo kabla zinatarajiwa kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato, kumwezesha mteja kudhibiti matumizi kulingana na anacholipia mteja, kupunguza na kudhibiti madeni ya maji pamoja na kupunguza malalamiko ya usomaji wa mita za maji. Katika awamu ya kwanza TUWASA imefunga jumla ya mita 400 eneo la Sikonge na Manispaa ya Tabora, zenye thamani ya shilingi 192,576,472 ambazo ni Miongoni wa shilingi 299,141,477.86 zilizotolewa na Serikali kutekeleza Mradi wa Ununuzi wa Dira za maji kwa ajili ya Mtandao wa maji Sikonge.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mhe. Upendo Wella ameeleza mradi huu ni kumuunga mkono Mhe. Rais kuhakikisha mteja anatumia kiasi alicholipia lakini pia kurahisisha ukusanyaji wa mapato kwa Taasisi.

