TAARIFA YA UTEKELEZA...
TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) SEKTA YA MAJI MJINI KALIUA-TABORA
12 Dec, 2023 Pakua

TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA ILANI YA CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) SEKTA YA MAJI KATIKA MJI WA KALIUA ILIYOTOLEWA KWA KAMATI YA SIASA YA MKOA WA TABORA TAREHE 11.12.2023

Ndugu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tabora na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Mzee Hassan Wakasuvi na Wajumbe wote wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Tabora, karibuni sana TUWASA, hasa katika Kanda ya Kaliua.

Ndugu Mwenyekiti wa CCM (M)

Mamlaka ya majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) inahudumia maeneo matano (5) ya Tabora Manispaa, Isikizya, Sikonge, Urambo na Kaliua.

Hali ya upatikanaji wa Maji katika maeneo hayo inatofautiana kutokana na uimara wa vyanzo vya maji. Tabora Manispaa na Isikizya ambazo zinatumia maji ya ziwa viktoria zina 95% ya upatikanaji wa maji hadi sasa. Mji wa Sikonge unapata maji kwa 40.5%, Urambo 24.5% na Kaliua 25%.

Ndugu Mwenyekiti wa CCM (M)

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) kupitia Tangazo la Serikali Na.788 la tarehe 03 Novemba 2023 imekabidhiwa rasmi kusimamia huduma ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Kaliua yenye kata tatu za Kaliua, Ushokola na Ufukutwa.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Mji wa Kaliua una wakazi 63,310. Chanzo cha maji katika Mji wa Kaliua ni visima virefu vilivyopo Kasungu, CHICO 5, CHICO 6, Mission, Stand, Ushokola na Usindi. Kutokana na ongezeko la haraka la watu katika mji wa Kaliua, mahitaji ya maji ni lita 4,558,000 kwa siku wakati uwezo wa uzalishaji maji ni lita 472,000 tu. Hivyo kuna upungufu wa huduma ya maji.

Ndugu Mwenyekiti wa CCM (M)

Ili kuboresha huduma ya maji katika maeneo ya Sikonge, Urambo na Kaliua, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa miji 28 kwa gharama ya shilingi Bilioni 143.26 ambapo Mkandarasi MEGHA ENGINEERING AND INFRASTRUCTURE LTD kutoka nchini India anaendelea na ulazaji wa bomba za kusafirisha maji ya ziwa Victoria kutoka Tabora Manispaa kupeleka miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua pamoja na maeneo ya Vijiji yaliyopo umbali wa mita 12 kutoka kwenye bomba kuu. Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 26 na umepangwa kukamilika tarehe 10 Oktoba 2025 au kabla. Mradi huu utakapokamilika utaongeza upatikanaji wa maji mjini Kaliua kutoka asilimia 25 hadi kufikia asilimia 95 iliyoelekezwa kwenye ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025.

Ndugu Mwenyekiti wa CCM (M)

Kwa mpango wa muda mfupi, Wizara ya Maji imetoa fedha shilingi Milioni 503.1 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa uboreshaji wa huduma ya majisafi na salama katika mji wa Kaliua ambao uliwekewa jiwe la msingi na Mhe. Jumaa H. Aweso (MB), Waziri wa Maji tarehe 29/07/2023 na baadaye kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru tarehe 18/09/2023. Mradi huu unafanya kazi vizuri na tayari kaya 110 zimeunganishiwa maji. Maelezo zaidi ya mradi yametolewa kwenye kiambatisho.

Ndugu Mwenyekiti wa CCM (M)

Naomba kuwasilisha

 

Eng. Mayunga A. Kashilimu

MKURUGENZI MTENDAJI-TUWASA