KERO YA MAJI URAMBO...
KERO YA MAJI URAMBO NA KALIUA KUFIKIA MWISHO, KALIUA KUWA MAMLAKA YA MAJI.
31 Jul, 2023
KERO YA MAJI URAMBO NA KALIUA KUFIKIA MWISHO, KALIUA KUWA MAMLAKA YA MAJI.

Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb) Waziri wa Maji (wa pili kutoka kushoto) amefanya ziara ya kikazi Kaliua na Urambo Tabora ambapo amekabidhi mradi wa Maji wa Miji 28 kwa mkandarasi kwa wilaya za Kaliua na Urambo pamoja na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa Kaliua.

Mhe. Jumaa Aweso baada ya kupokea taarifa fupi ya hali ya huduma ya maji Manispaa ya Tabora amesema hana wasiwasi na utendaji wa TUWASA wala RUWASA pia ametoa pongezi nyingi kwa watumishi wa Wizara ya Maji Tabora kwa namna ambavyo wanawahudumia wananchi.

Amewaagiza wataalam kuhakikisha wanafanya utafiti ili kuleta maji Ulyankulu Mara baada ya maji hayo ya Ziwa Victoria kufika Kaliua kupitia mradi wa maji wa miji 28 unaotarajiwa kukamilika kabla ya mwaka 2025 na kumaliza changamoto ya maji Kaliua na Urambo.

Aidha kipekee amempongeza Eng. Mayunga Kashilimu Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA kwa utekelezaji mzuri wa mradi wa Kaliua na amemuongezea jukumu la kusimamia  Kaliua kwa huduma ya maji kwani ni mji unaokua sana na pia itasaidia wananchi kupata huduma ya majisafi na ajira kwa wakaazi wa Kaliua zitapatikana.

Pamoja na hayo amesisitiza TUWASA ihakikishe haipigi danadana wateja wanapoomba kuungwa kwene huduma, bili zisiwe bambikizi, wateja washirikishwe katika kusoma Dira za maji na pia wananchi waulinde mradi kwani ni jukumu lao la msingi.

"Bisheni hodi mtafunguliwa" Mhe. Jumaa Hamidu Aweso.

Mhe. Jumaa Aweso ameyasema hayo baada ya mkuu wa wilaya ya Kaliua Dkt Rashid Chuachua kumshukuru kwa miradi ya maji na kumuomba ikimpendeza awape TUWASA waisimamie Kaliua na RUWASA waendelee kusimamia maeneo mengine ya vijijini.