BODI YA WAKURUGENZI...
BODI YA WAKURUGENZI TUWASA YASISITIZA MRADI WA MAJI MIJI 28 UKAMILIKE KWA WAKATI WANANCHI SIKONGE, URAMBO NA KALIUA – TABORA WAPATE MAJI.
13 Aug, 2025
BODI YA WAKURUGENZI TUWASA YASISITIZA MRADI WA MAJI MIJI 28 UKAMILIKE KWA WAKATI WANANCHI SIKONGE, URAMBO NA KALIUA – TABORA WAPATE MAJI.

Bodi ya Wakurugenzi – TUWASA inayoongozwa na Bw. Dick Mlimuka  imepokea taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Miji 28 kupeleka maji Sikonge, Urambo na Kaliua kutoka kwa Mhandisi Mayunga A. Kashilimu ambaye ni katibu wa Bodi hiyo ambaye ameeleza kuwa mradi huu umefikia asilimia 71.2 ya utekelezaji hadi mwezi Julai,2025 ambapo umeanza kutekelezwa tarehe 11.04.2023 na utakamilika baada ya miezi 30 chini ya Mkandarasi Megha Engineering and Infrastructure Ltd na Mhandisi Mshauri  WAPCOS Ltd. Wenye thamani ya shilingi Bilioni 143.26.

Ameendelea kueleza  kuwa miji hiyo mitatu ina mahitaji ya maji lita 9,739,000 na mradi ukikamilika utazalisha maji lita 24,760,000 kwa wilaya zote tatu na wananchi 490,926 watanufaika na mradi huu ikihusisha na vijiji 63 vilivyopo njiani mabomba yanapopita.

Bodi hiyo imetembelea mradi Sikonge na Urambo kisha  imemsisitiza mkandarasi kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora na kwa wakati yaani Octoba 2025 ukamilike, mabomba km 21 kwa ajili ya Urambo na Kaliua yafuatiliwe na kuwasili haraka ili mradi uendelee kutekelezwa na vifaa vyote vinavyotakiwa viagizwe ili isitokee upungufu wa vifaa na kuchelewesha mradi.

Mhandisi Mshauri WAPCOS LTD amethibitisha kuwa mradi utakamilika Octoba 2025 baada ya mabomba km 21 kuwasili mwezi Septemba, 2025. Ameongeza kuwa wataalam wa Wizara ya maji na KASHWASA wapo Nchini India kwa ajili ya ukaguzi wa mabomba yanayotarajiwa kuletwa kwa ajili ya Urambo na Kaliua.