KAMATI YA USALAMA YA...
KAMATI YA USALAMA YA WILAYA YA SIKONGE YATEMBELEA BWAWA LA UTYATYA KUONA HALI YA BWAWA
02 Nov, 2023
KAMATI YA USALAMA YA WILAYA YA SIKONGE YATEMBELEA BWAWA LA UTYATYA KUONA HALI YA BWAWA

Kamati ya Usalama ya Wilaya ya Sikonge ikiongozwa na Kaimu Mkuu wa Wilaya Bi Faraja Mwakyoma (wa pili kutoka kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri, Waheshimiwa Madiwani na Kaimu mkurugenzi mtendaji wa TUWASA leo tarehe 02.11.2023 wametembelea bwawa la UTYATYA kuona hali ya bwawa lilivyopungua kina cha maji na kuleta changamoto ya huduma ya maji mjini Sikonge.

Kaimu mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA Ndugu Bernard Biswalo ameeleza changamoto ya kukauka kwa bwawa hilo inavyoathiri hali ya huduma ya maji kwa wakaazi wa Sikonge na kueleza mikakati iliyopo kama ifuatavyo;-

Mkakati wa dharura wa uchimbaji wa visima vitatu kwa maeneo ambayo yamefanyiwa utafiti na yameonekana yana maji ya kutosha baada ya mkakati wa kuchimba mtaro na kusogeza mabomba na pampu ili kuvuta maji bwawani kushindwa kufanya kazi kutokana na kukauka.

Utekelezaji unaoendelea wa mradi wa maji ya Victoria kutoka Tabora kuja Sikonge ambapo Tenki la maji la lita 1,000,000 limeanza kujengwa.

Sambamba na maelezo ya Kaimu Mkurugenzi wa TUWASA, Eng. Respicious Mushobozi (wa pili kutoka kulia) wa Ofisi za Bonde la Ziwa Tanganyika ameeleza kuwa Bwawa hili kwa kiasi kikubwa limeathiriwa na shughuli za kibinadamu ingawa lilijengwa mwaka 1958 na mabwawa huwa yanadumu kwa miaka 40 hadi 50.

Bwawa limejaa mchanga lakini pia matumizi ya maji yameongezeka hivyo kwa dharura wataondoa tope bwawani hapo ili kuongeza kina cha maji na mwaka 2024 baada ya masika kuisha utafanywa ukarabati mkubwa wa bwawa hili.

Kaimu mkuu wa Wilaya ya Sikonge amewaagiza TUWASA kuharakisha mpango wa dharura wa kusaidia wananchi kupata maji kwa haraka kama vie kutumia magari ya majisafi kusambaza maji kwa wananchi licha ya mikakati aliyoieleza kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji amepokea maelekezo hayo na kusema yeye pamoja na Menejimenti ya TUWASA wataanza kufanya utaratibu wa magari ya majisafi wakati mikakati mingine ikiendelea kutekelezwa na kwamba tuendelee kuomba mvua inyeshe mapema ili bwawa la UTYATYA lipate maji ya kusambaza kwa wananchi.