WIZARA YA MAJI YAIKO...
WIZARA YA MAJI YAIKOSHA KAMATI YA BUNGE USHIRIKISHAJI WANANCHI MIRADI YA MAJI
05 Feb, 2024
WIZARA YA MAJI YAIKOSHA KAMATI YA BUNGE USHIRIKISHAJI WANANCHI MIRADI YA MAJI

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imeipongeza Wizara ya Maji kwa ushirikishaji wananchi wakati wa kutekekeza Miradi ya maji.

Pongezi hizo zimetolewa Mkoani Tabora baada ya Kamati hiyo kutembelea Mradi wa maji wa miji 28 kwa mji ya Sikonge, Urambo, Kaliua na Uyui ambapo ulazaji mabomba umbali wa kilometa 111.22 kuelekea katika miji hiyo unaendelea.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) amesema ushirikishwaji wa wananchi ni mzuri kwani huondoa malalamiko na kuwezesha miradi kukamilika kwa haraka na kwa wakati.

Akiwasilisha taarifa ya Mradi Mratibu wa Mradi huo Mhandisi Edward Tindwa, ameelezea changamoto wanayokutana nayo kwa sasa ni kilimo ambacho kinaendelea katika maeneo unakopitia Mradi.

"Mara zote   wananchi wanashirikishwa na wanatoa ushirikiano na kuruhusu mabomba ya maji kupita" amesema.

Aidha, Kamati hiyo imesisitiza suala la utunzaji wa miundombinu ya maji na kuhakikisha maji yanayozalishwa na Miradi hiyo yanasambazwa kwa wananchi.

Pamoja na mambo mengine Kamati imetembelea Mradi wa Ukarabati wa Bwawa la Igombe na kuridhishwa na utekekezaji wake.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maji Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Wizara inaendelea na jitihada ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi wote.

 "Kukamilika kwa mradi wa maji wa Miji 28 Mkoani hapa kutawezesha huduma ya maji kutoka ziwa Victoria kuzifikia wilaya zote za Mkoa wa Tabora na tutaendelea kusimamia ili kuhakikisha Watanzania wote wananufaika na huduma ya majisafi na salama" amesema Mahundi

Bwawa la maji la Igombe limekarabatiwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 1.7 na limekamilika kwa asilimia mia moja na mradi wa miji 28 unatekelezwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 143.26 unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2025.