BODI YA WAKURUGENZI...
BODI YA WAKURUGENZI YA KASHWASA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI KUTOKA ZIWA VICTORIA WENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 145.7 TABORA.
09 Aug, 2024
BODI YA WAKURUGENZI YA KASHWASA YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA  MRADI WA MAJI KUTOKA ZIWA VICTORIA WENYE THAMANI YA SHILINGI BILIONI 145.7 TABORA.

Bodi ya Wakurugenzi ya KASHWASA imekagua utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuja Miji ya Sikonge, Urambo na Kaliua ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 45 na imeridhishwa na utekelezaji.

Mwenyekiti wa Bodi ya KASHWASA Mha. Joshua Mgeyekwa amesema kwamba wameona ujenzi wa matenki matano ukiendelea pamoja na shughuli zote za ujenzi na kujiridhisha kuwa mradi huu utakamilika ndani ya muda uliopangwa na ameishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa – Tabora kwa ushirikiano wake kwa wakandarasi katika utekelezaji wa Mradi huu na kumhakikishia kuwa Bodi ya KASHWASA itaendelea kusimamia kikamilifu mradi huu kwani utakapokamilika utachochea maendeleo kiuchumi.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TUWASA ndugu Benard Biswalo baada ya kuwasilisha taarifa ya utendaji ya TUWASA ameshukuru kwa ziara ya Bodi ya KASHWASA na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa – Tabora kwa ushirikiano anaouonesha katika mradi huu na ni matarajio kuwa mradi huu utatekelezwa kwa wakati na  kwa kuzingatia thamani ya fedha.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt.Rogath Mboya ameipongeza Bodi hii kwa kuthibitisha kuwa  Mradi huu utakamilika kwa wakati kwani unagusa maisha ya wanaTabora kwa kiasi kikubwa na ametaka kuhakikisha Mradi huu unakamilika kabla ya Octoba, 2025.

Pia mkandarasi wa Mradi huu kampuni ya M/S Megha Engineering Infrastructur LTD ameeleza kuwa kwa hapa utekelezaji wa mradi ulipofikia ni wazi kabisa utakamilika ndani ya muda wa mkataba au kabla ya muda ambao ni Octoba, 2025.

Mhe. Paul Chacha Mkuu wa Mkoa wa Tabora amewapongeza wakandarasi wa mradi huu kwa utakelezaji wenye matumaini makubwa na amesema Ofisi yake ipo tayari muda wowote kusaidia  na kuhakikisha mradi huu mkubwa wa Serikali unakamilika kwa wakati. “Tunawaombea kila lakheri na afya njema kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati” Mhe. Paul Chacha.