KIKAO CHA BARAZA LA WAFANYAKAZI TUWASA KIMEKETI LEO TAREHE 12.02.2025.

Kama ilivyo kawaida ya vikao vya Baraza la Wafanyakazi kuketi kwa ajili ya kushauri namna bora ya uendeshaji wa Mamlaka, leo kimeketi kikao hicho kwa ajili ya kujadili mapendekezo ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/26 yaliyowasilishwa na Bw. Innocent Hunja ambaye ni Mkuu wa kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini TUWASA.
Kikao hicho kimeongozwa na Kaimu Mwenyekiti Bw. Benard Biswalo na ameshiriki muwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Maji Bi Sofia Swai na Katibu wa Tughe (M) Bi Amina Mwaluko.
Wajumbe wameshauri bajeti iweke kipaumbele kwenye kuongeza mapato ikiwepo kupunguza upotevu wa maji, kurudisha wateja waliokatiwa maji, kuongeza wateja wapya na kufuatilia matumizi ya maji.
Pia watumishi wazingatiwe kuhusu maslahi na wapewe elimu kuhusu huduma kwa mteja.
Bi Amina Mwaluko, ameiomba Wizara ya maji kusaidia TUWASA hasa maeneo ya Sikonge, Urambo na Kaliua ili kukidhi gharama za uendeshaji kipindi hiki ambacho mradi wa miji 28 unasubiriwa kukamilika.
Aidha mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya maji alieleza kwamba, suala la upotevu wa maji lipewe kipaumbele sambamba na TUWASA kupeleka Wizarani maandiko mbalimbali ya kuainisha miradi ambayo itasaidia kuboresha huduma na kuongeza mapato kisha Wizara itakua inaangalia namna bora ya kusaidia.
Kaimu Mwenyekiti aliwahoji wajumbe kama wameipitisha bajeti iliyowasilishwa na walikubali kuipitisha pamoja na mapendekezo ya Baraza.
Mwisho kabisa Kaimu Mwenyekiti Bw. Biswalo alihitimisha kwa kuiomba Wizara itoe kipaumbele TUWASA kuhusu gharama za usambazaji wa mtandao wa maji Sikonge, Urambo na Kaliua baada ya mradi wa miji 28 kukamilika Octoba, 2025.