UTUNZAJI WA VYANZO VYA MAJI KATIKA KIPINDI CHA MEZA HURU KUPITIA REDIO VOT
Leo tarehe 09.11.2023 katika kipindi cha meza huru kupitia VOT FM Bi Najibah Batenga Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma amezungumza kuhusu Utunzaji wa Vyanzo vya Maji kama vile mabwawa, maziwa, bahari na maji chini ya ardhi. Pia ameeleza kwamba ni muhimu kutunza na kulinda vyanzo hivyo kwa ajili ya vizazi vya sasa na baadae kwa kuacha kufanya shughuli za kibinadamu katika maeneo ya vyanzo kama vile kilimo,ukataji wa miti, ufugaji na unyweshaji wa mifugo katika vyanzo vya maji.
Ameendelea kueleza kwamba ni vizuri zifanyike shughuli ambazo ni rafiki wa mazingira na vyanzo vya maji kama vile ufugaji wa nyuki n.k kwakuwa kutofanya hivyo kunapelekea mabadiliko ya tabia nchi kwa kuongezeka kwa joto linalopelekea kupungua kwa maji au kukauka kabisa na pia kupungua kwa ubora wa maji ambao unasababisha matumizi ya gharama kubwa za kusafisha na kutibu maji ili yasambazwe kwa wateja yakiwa safi na salama.
Ametoa wito kwa wadau wa maji kila mmoja kuwa balozi na mlinzi wa mwenzake katika kulinda na kutunza vyanzo vya maji kwani maji ni uhai, maji ni ustaarabu na pia maji ni uchumi, lakini pia amemalizia kwa kuwakumbusha wateja kuwa na utaratibu wa kukinga na kuhifadhi maji na kisha kulipia bili zao kwa wakati.