KUNDO AKAGUA MIRADI YA MAJI TABORA AWATAKA WANANCHI KUTUNZA MIUNDOMBINU YA MAJI

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Kundo Mathew, amewaomba wabunge katika majimbo yao kuhakikisha wanashirikiana na wananchi katika kutunza miundombinu ya maji ili miradi inayozinduliwa iwe endelevu.
Mhandisi Kundo ameyasema hayo Machi mosi, 2025 Mkoani Tabora wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya maji mkoani Tabora, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya mijini na vijijini.
Mhandisi Kundo amefika Mkoani Tabora na kupokelewa na Cornel L. Magembe, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ambaye alimuonyesha taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji katika mkoa wa Tabora.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tabora, Mhandisi Hatari Kapufi, upatikanaji wa maji katika maeneo ya mijini umefikia asilimia 70, huku vijijini ukiwa ni asilimia 68.2.
Katika ziara yake, Mhandisi Kundo amekagua miradi mbalimbali ya maji, ikiwemo mradi wa Nyampindi kijiji cha Mpumbuli wilayani Uyui, ambao utakapokamilika mwaka 2025, utafaidisha wakazi 10,247 ambapo hadi sasa, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 50.
Aidha, amekagua ujenzi wa bwawa la maji la Kizengi wilayani Uyui, ambalo linatarajiwa kunufaisha wakazi 90,000 ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 60.
Mhandisi Kundo pia amekagua mradi wa maji wa Mpumbuli - Nzega Vijijini, ambao pia unatarajiwa kunufaisha wakazi wa eneo hilo.
Kwa upande wake Dkt. Rogath Mboya, ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, amewashukuru wadau wa sekta ya maji kwa ushirikiano wao, akisisitiza umuhimu wa Wizara ya Maji kufuatilia madeni ya taasisi ili kuhakikisha sekta hii inajiendesha vema.
Kwa upande mwingine, Cornel Magembe, ambae ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuleta miradi ya maji Mkoani Tabora, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Mhandisi Kundo ameeleza umuhimu wa kuhakikisha kuwa miradi yote inakamilika kwa wakati ifikapo Juni, 2025, ili wananchi waweze kupata huduma kwa wakati.