Mhe. WASIRA AFURAHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA MAJI MIJI 28 TABORA.

Mhe. Stephen Masatu Wasira - Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania ametembelea Mradi wa maji wa miji 28 Tabora ambapo amepata maelezo kuhusu utekelezaji wa mradi huo ambao umefikia asilimia 69.
Eng. Mayunga Antony Kashilimu - Mkurugenzi Mtendaji TUWASA aliwasilisha taarifa ya mradi katika kijiji cha Muungano wilaya ya Urambo iliyoonesha kuwa mradi huu unatekelezwa na mkandarasi Megha Engineering and Infrastructure Ltd na Mhandisi Mshauri WAPCOS LTD.
Aidha, ameeleza kwamba mradi huu unagharimu fedha za kitanzania shilingi bilioni 143.26 na unatarajiwa kukamilika Oktoba , 2025 na kuhudumia wakazi wa Urambo, Kaliua na Sikonge.
Eng. Kashilimu amesema mradi huu utanufaisha wakaazi 490,926 na upatikanaji wa maji utafikia asilimia 95 utakapokamilika mradi na uzalishaji wa maji utafikia lita 24,760,000 dhidi ya mahitaji ambayo ni lita 9,739,000 kwa miji yote mitatu.
Mhe. Wasira amepongeza na kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huu kwa kuwa anatambua changamoto ya maji kwenye miji hii na hakika changamoto hiyo itakwisha.
Mhe. Wasira amesema Serikali ya CCM ina sifa ya kusema na kutenda kama ilivyo maamuzi ya kuleta maji ya Ziwa Victoria yanavyotekelezwa na Mradi unaendelea.
Amemalizia kwa kusema Kauli mbiu ya Mhe. Rais ni kumtua mama ndoo kichwani ndio maana miradi mingi ya maji inatekelezwa nchi nzima.
Amewataka wananchi wote baada ya kukamilika mradi huu wakapata maji safi na salama wawe na kazi moja tu ya kuyalipia maji.